Mabingwa
watetezi wa ligi kuu Tanzania bara timu ya Yanga imeendeleza wimbi la
ushindi katika kuhakikisha inalitetea vyema taji lake baada ya leo kutoa
kipigo kingine cha goli 3-0 mbele ya Tanzania Prisons ‘wajelajela’
kutoka jijini Mbeya kwenye mtanange uliomalizika jioni ya leo kwenye
uwanja wa Taifa.
Yanga
walianza kupata goli la kwanza kipindi cha kwanza kupitia kwa Mbuyu
Twite aliyemalizia mpira uliomponyoka mlinda mlango wa Prisons Mohamed
Yusuf na kumkuta Twite aliyeachia shuti kali akiwa hatua chache kutoka
langoni.
Wakati
ikiwa imeongezwa dakika moja ya nyongeza ili mchezo kwenda mapumziko,
Amis Tambwe aliifungia Yanga bao la pili baada ya golikipa Mohamed Yusuf
kuutema mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na kiungo wa Yanga Thabani
Kamusoko na Tambwe kumalizia kwa kichwa na kuifanya Yanga kwenda
mapumziko ikiwa mbele kwa goli 2-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa Tanzania Prisons kumpumzisha golikipa wao Mohamed Yusuf na kumuingiza Aron Kalambo.
Mshambuliji
wa Yanga Donald Ngoma aliihakikishia Yanga ushindi mnono kwa kufunga
mkwaju wa penati kufuatia James Josephat kumchezea vibaya Simon Msuva
kwenye eneo la hatari. Kutokana na Josephat kumfanyia madhambi Msuva,
mwamuzi aliizawadia Yanga mkwaju wa penati pamoja na kumtoa nje Josephat
kwa kadi nyekundu.
Huo
unakuwa ni ushindi wa pili mfululizo kwa klabu ya Yanga baada ya
kushinda mchezo wake wa awali kwa goli 2-0 dhidi ya Coastal Union kwenye
uwanja huohuo wa Taifa wakati Tanzania Prisons wao wamepoteza michezo
yote miwili waliyocheza jijini Dar es Salaam. Walifungwa goli 2-1 na
Azam FC kwenye uwanja wa Azam Complex kabla ya leo kuchezea kichapo cha
goli 3-0 mbele ya Yanga.
Mashabiki wa Yanga wakiwa wamepagawa baada ya timu yao kuvuna pointi tatu muhimu kwenye mchezo dhidi ya Tanzania Prison
0 comments