BODI ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar,
imeagizwa kuacha mara moja upendeleo wa kutoa mikopo kwa watoto wa
vigogo kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na malengo ya kuanzishwa
kwa taasisi hiyo.
Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Seif
Sharif Hamad alitoa agizo hilo jana alipozungumza na uongozi na
watendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar Mnazi Mmoja mjini
hapa.
Seif alisema yapo malalamiko mengi
kutoka kwa wananchi na wazazi, kwamba Bodi hiyo inatoa mikopo kwa watu
ambao hawana sifa, wakiwamo watoto wa vigogo.
“Yapo malalamiko mengi ya wananchi na
wazazi kuhusu Bodi hii, ikiwamo kutoa mikopo kwa njia ya upendeleo kwa
watu ambao hawana sifa na watoto wa wakubwa,” alisema.
Alikumbusha watendaji wa Bodi hiyo,
kwamba taasisi hiyo imeanzishwa kusaidia maendeleo ya watoto masikini
wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za masomo.
“Hayo ndiyo malengo ya kuanzishwa kwa
Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, kutoa mikopo kwa watoto wa masikini
wasiokuwa na uwezo wa kugharimia masomo,” alisisitiza.
Alisema wakifanikiwa kutekeleza malengo
hayo kwa kiasi kikubwa, Bodi itatoa mikopo kwa wanafunzi wengi na
kuepusha urasimu na kutiwa shinikizo kutoka kwa wakubwa.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo,
Iddi Khamis alisema Bodi imezidiwa na maombi na mahitaji ya wanafunzi wa
elimu ya juu wanaohitaji mikopo hiyo wakiwamo wenye sifa.
Akifafanua, Iddi alisema kwa sasa vipo
vyuo vya elimu ya juu vinne vikiwa na wanafunzi wenye mahitaji ya mikopo
kwa ajili ya kujiendeleza zaidi, lakini Bodi haina uwezo huo.
“Tumezidiwa na idadi ya wanafunzi
wanaohitaji mikopo ya elimu ya juu sasa…vipo vyuo vikuu vinne vyenye
wanafunzi wanaohitaji mikopo,” alisema.
Hata hivyo, Khamis alisema kwa bajeti ya
mwaka 2012/13, Bodi imeongezwa bajeti ya fedha kutoka Sh bilioni 4 hadi
Sh bilioni 8 ingawa bado hazitoshi.
Alifafanua, kuwa maombi ya mikopo kwa
wanafunzi yameongezeka kutoka 800 hadi 1,800 na Bodi imeshindwa kuwapa
mikopo wanafunzi hao wa ziada hivi sasa.
Hata hivyo, wanafunzi wanaokosa mikopo
kutoka Bodi hiyo bado wana nafasi ya kuomba kupitia Bodi ya Mikopo ya
Elimu ya Juu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
0 comments