UONGOZI
wa Serikali ya wanafunzi wa Chuo cha Usimamazi wa Fedha (IFMSO) cha
jijini Dar es Salaam, umesema hali ya usalama kwa sasa katika Hosteli za
Kigamboni inaridhisha.
Waziri
Mkuu wa IFMSO, Daniel Sarungi alisema jana kuwa tangu iundwe timu ya
polisi inayoshirikiana na wanafunzi hao hali imekuwa tulivu kwa kipindi
cha wiki moja iliyopita.
Sarungi alisema kuwa hakujatokea uvamizi tena
katika hosteli zao, lakini akaongeza kusema kuwa taarifa kamili ya
ripoti ya timu hiyo itatolewa na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya
Mkoa wa Dar es Salaam, Suleiman Kova.
“Kuna amani sana, misako imefanyika lakini ripoti itatolewa Januari 30 na Kamanda Kova,” alisema Sarungi.
Kauli
ya Kiongozi huyo wa wanafunzi haikutofautina na ya Kamanda wa Polisi
mkoa wa Temeke, Englbert Kiondo, ambaye alisema taarifa inayohusu hali
ilivyo itatolewa na Kamanda Kova.
Kwa upande wa wakazi wa Kigamboni, walisema kuwa wameshuhudia polisi wakifanya doria maeneo hayo tofauti na ilivyokuwa huko nyuma kabla wanafunzi hawajaandamana.
Walisema
pia wameona polisi wakiwakamata wahalifu kwenye maeneo hayo kutokana na
misako wanayoifanya hali ambayo imeleta utulivu kwenye mji huo.
Naye
mkazi mwingine anayejishughulisha na biashara ya kioski, alisema kuwa
kumekuwa na utulivu kwani hata wanafunzi ambao ndiyo wateja wake wakubwa
wanamwambia kuwa wanaweza kuacha vitu wakavikuta salama.
0 comments